Kuzuia madhara ni muhimu zaidi kuliko kujipatia maslahi / manufaa
Question
Je, kupigana na wasio Waislamu katika zama za kisasa kunawapatia Waislamu maslahi kama wanavyodai wenye fikra potofu?
Answer
Miongoni mwa misingi ya Sharia iliyo thabiti kuwa: "Kuzuia madhara ni muhimu zaidi kuliko kujipatia maslahi" na msingi huu unao umuhimu mkubwa mno, ambapo matendo ya watu ama huwa na heri / manufaa au shari, kwa hiyo Waislamu wanapaswa kuangalia kwa makini na kupima mambo vizuri kabla hawajafanya chochote, ili heri ionekane na kudhihiri, na la msingi ni kwamba kuzuia madhara ni muhimu zaidi kuliko kujipatia manufaa, kwa dalili nyingi kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Aya zake mpate kufikiri} [Al-Baqarah: 219].
Maana ya Aya ni kuwa ulevi na kamari vilikuwa na manufaa kwa baadhi ya watu, lakini vimeharamishwa kwa kuwa madhambi yanayopatikana kwavyo ni mengi zaidi.
Kanuni hii ya "Kuzuia madhara ni muhimu zaidi kuliko kujipatia manufaa" ni maarufu kwa wanafiqhi, madhara yakipingana na manufaa, basi katika hali hii kuzuia madhara huwa muhimu zaidi, kwani sharia inajali makatazo zaidi kuliko maagizo, kwa hiyo Mtume (S.A.W.) amesema: "Nikiwaagizeni jambo basi mlifanye kadri mtakavyoweza, na nikiwakatazeni jambo, mliache kabisa".
Jihadi kwa maana yake ya kisasa – tukikubali kuiita Jihadi, kwani vitendo vya makundi ya kigaidi ni ugaidi siyo Jihadi – huambatana na kumhukumu mtawala ukafiri kwa visingizio mbalimbali, jambo linalochafua taswira ya Uislamu, hukumu zake na wafuasi wake kimakusudi, na kupelekea madhara mengi na kuchochea vita na migogoro mingi ambayo Waislamu pengine hawataweza kujitetea, hivyo, ugaidi ambao makundi yenye fikra potofu wanauita "Jihad" unayo madhara mengi zaidi kuliko manufaa.