Hadithi Dhaifu na Maudhuu
Question
Ni ipi Hadithi dhaifu na kuna tofauti gani kati yake na Hadithi maudhuu, na je inajuzu kutekeleza yanayokuja katika Hadithi dhaifu, na katika hali gani?
Answer
Hadithi dhaifu ni ile Hadithi iliyokosa sharti moja au zaidi miongoni mwa masharti ya Hadithi Sahihi au iliyo hasan, na Hadithi dhaifu huwa hivyo kwa kupatikana kasoro kuhusu umakini wa msimuliaji wake si kwa uadilifu wake, kwani msimuliaji aliye na kasoro kuhusiana na uadilifu wake hakubaliki kabisa ambapo huwa sawa sawa na mwongo na anayetunga maneno akadai kuwa ni Hadithi, na anayesema uongo kuhusu Hadithi za Mtume (S.A.W.) ni mtu hatari aliahidiwa adhabu kubwa kwa mujibu wa kauli yake Mtume: "Yeyote anayesema uongo kuhusu Hadithi zangu, basi ajiandae kuingizwa motoni" (Imekubalika kwa wote).
Wataalamu wanaona kuwa msimuliaji wa Hadithi akiwa na kasoro ndogo katika umakini wake wa kusimulia Hadithi, basi ni jambo ambalo linaweza kurekebishwa kwa njia ya kutafuta msimuliaji mwingine aliye makini ikawa Hadithi yenyewe ni sahihi au hasan kwa mwingine, hivyo huwa ni Hadithi inayokubalika kuwa chanzo cha hukumu ya kisharia ikihitajika, nayo Hadithi dhaifu hukubalika katika mazuri kwa jumla, kama vile kuhofisha kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa wahalifu, na kupendezesha kwa kutaja malipo mazuri au adhabu iliyotajwa katika vyanzo vinginevyo kama upole kwa wazazi, tasbihi, dhikri na kadhalika.
Ama Hadithi maudhuu ambayo Mtume (S.A.W.) hakuisema kabisa, basi ni aina ambayo kasoro zake hazirekebishwi hata kidogo na wala haijuzu kusimuliwa ila kwa ajili ya kufafanua uongo wake, bila ya kuzingatiwa katika hukumu za kisharia wala mambo mazuri katika dini.