Hadithi: Nimeamrishwa kupigana na watu
Question
Watu wengi wenye misimamo mikali huegemeza mashambulizi yao kwa watu kwenye Hadithi “Nimeamrishwa kupigana na watu.” Je! Hadithi hii ni sahihi? Na ina maana gani?
Answer
Hadithi imekubaliwa na ina mapokezi mengi. Neno la “Watu” hakika halimaanishi watu wote, na hakuna shaka kwamba Mu’ahid na wasiokuwa Waislamu wametengwa na Hadithi hii. Kwa mujibu wa kauli yake Mtume, (S.A.W): “Mwenye kumuuwa muahadi hatasikia harufu ya Pepo, ingawa harufu yake inanukia kwa umbali wa miaka arobaini.” Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari.
Lakini wale watu wanaoanzisha uchokozi na kupigana dhidi yetu, Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuwazuie na kurudisha uchokozi wao; Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: “Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui.” [Al-Baqarah: 190] Kwa hiyo, Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema katika Hadithi hii: “Nimeamrishwa nipigane na watu,” maana yake: anayefanya uadui. Na Mtume (S.A.W) ameamrishwa, na aliyemwamrisha ni Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Hadithi hii imethibitishwa na Hadithi nyingine isemayo: “Nimeamrishwa kupigana na washirikina.”
Na ama wale wasiotupigania, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuamrisha kuwafanyia wema na kuwafanyia uadilifu. Mwenyezi Mungu akasema: “Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.” (Al-Mumtahanah: 8).
Wale wasiotupiga vita tutakuwa wapole kwao na tutakuwa waadilifu, na tutawaacha kwenye dini yao wala hatutawashambulia.
Mwenye kuifahamu Hadithi isiyokuwa hiyo tuliyoitaja basi huyo ni mtu mwenye fitna, anataka kuhalalisha kuuwa kwake watu wote, au anataka kutilia shaka Sunna ya Mtume (S.A.W).